How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 13 August 2014

Kijiwe chaunda UKAWA na Akawo chalaani tuzo

BAADA ya matumaini ya kupatikana Katiba mpya kupotea kutokana na woga na ujinga wa baadhi ya wadau wasiotaka kuutema ulaji, Kijiwe kimeamua kuingilia kati kukwamua mchakato tena kwa bei nafuu na mawazo bora.
Msomi ndiye anayeanzisha mapinduzi haya yatakayoikomboa kaya toka kwenye mikono michafu ya manyang’au wa Chama Cha Mafisi na Mafisadi (CCMM) kinachotaka kuhakikisha katiba mpya haiandikwi ili kiendelee kuhomola na kucheza mahepe kwa wachovu.
Anakula mic, “Jamani, mnaonaje huu mkwamo wa Katiba mpya unaosababishwa na wapuuzi wanaodhani kuwa wao ndiyo wameumbwa kuwatawala na kuwala wenzao?”
Mijjinga hangoji, “Naona hapa msomi umelenga mle mle mtakiwamo kulengwa. Lazima vidume tuingilie kati kuhakikisha tunapata Katiba yetu tena mwaka huu kabla ya uchakachuaji mwakani.”
Mgosi Machungi ambaye amenunua kisimu kipya anachopenda kubofya bofya anakula mic, “Ni kwei. Lazima tiamke na kuwaonyesha hawa matwahuti kuwa hii kaya ni yetu. Lazima tiwatimue huko Idodomya ili kupata katiba mpya.”
Mpemba hajivungi. Anakwanyua mic, “Yakhe haya mawazo ya kimapinduzi kweli.  Kwanini turuhusu wahuni wachache na wezi waamue hatima yetu? Tutamke wazi kuwa tunataka katiba mpya na lazima tuiandike wenyewe kulingana na rasimu ya Waryoba watake wasitake.”
“Lazima kijiwe kionyeshe kuwa ni icon of democracy and constitution tofauti na wazushi wanaosifiwa upuuzi wakati wameharibu kila kitu kana hamnazo.”
“Mmeipata ya jamaa yetu Mpenda Sifa Njaa Kaya alivyoongezewa ujiko uchwara asijue ameingizwa mkenge na matapeli wa kinigeria kwa kupewa tuzo mawenge?”Anauliza Mbwamwitu kwa masihara.
“Unaongelea mauzauza ya icon of demoncrazy siyo?”Anauliza Kapende. “Usinichefue. Hivi na mkwamo huu wa Katiba bado kuna wapumbavu wanaodhani wachovu ni wapumbavu kama wao wampe mtu tuzo? Kama ni tuzo basi iwe ni tuzo ya kuvurunda lakini si kufanya lolote wala chochote cha maana.” Anang’aka mheshimiwa Bwege.
“Nshawaambia hii ni demoncrazy award wallahi. Nadhani walikosea kuita icon of democracy badala ya icon of demoncrazy.” Anazoza Mpemba.
“Wenzenu wanasuka mbinu ya kuingilia na kupata ulaji wa dezo kwenye shamba la chizi nyie mnalalamika?” Anachomekea  Mipawa aliyekuwa akijiserfie.
“Yakhe mie naona hii tuzo ingepaswa tupewa sisi wanakijiwe kama kweli ingekuwa tuzo. Kwa vile ni aibu na matusi basi alopata yamfaa sema kosa waloitoa ni kuiita ya demokrasi ati.” Mpemba anakatua mic tena.
“Nadhani hawakukosea. Ukiangalia mauaji ya Arusha, uchakachuaji, EPA, kutesa wambea wa vyombo vya umbea, akina Ulimbwoka unategemea nini kama hili si suto?”
Sofia Lion aka Kanungaembe hakubaliani na mawazo ya wenzake. Anakwanyua mic, “Hivi nyie watu mfanyiwe nini ndiyo mridhike? Mmeambiwa ni tuzo ya icon of democracy mnaanza lawama. Hivi hamuoni tulivyo na demokrasi hadi kila mtu anasema atakacho?”
“Demokrasia ya kweli si kusema hovyo wala kuruhusu kusema hovyo bali kutenda haki na mambo yanayoingia akilini. Hivi kweli kiongozi wa kaya inayoajiriana kwa ukoo na kujuana anaweza kuwa icon of democracy au icon of demoncrazy?” Msomi anazidi kukandia.
“Tena umetikumbusha Msomi. Azima tuunde Umoja wa Katiba ya Wanakijiwe (UKAWA) ili kusaidiana na UKAWA ya wanasiasa tukomboe kaya yetu.” Anazidi kumwage pwenti Mgosi Machungi.
“Mgosi wankuna hapa. Lazima tuunde na Umoja wa Ajira kwa Wote (AKAWO) ili kupambana na vinyangarika na vichimbakwiri wanaotumia madaraka kwa manufaa yao ati.” Mpemba naye anazidi kupagawisha kijiwe.
“Tena tikitoka hapa azima twende Uhamiaji na kuhakikisha wae wote waioajiri ndugu zao wanakamatwa na kutupwa upango haaka.” Ananguruma Mgosi huku akishangiliwa kwa pwenti zake.
Msomi anapoka mic na kudema, “Napendekeza: Mosi, Bunge Maalum la Katiba (BMK) livunjwe na wabunge warejeshe njuluku zetu. Pili, tuunde BMK isiyo ya ulaji ambapo wahusika watalipwa njuluku laki moja kwa siku na kuhakikisha wanapewa muda maalum wa kuandika katiba. Tatu, mkuu apigwe marufuku kuingilia wala kuongelea mchakato kwa vile amechemsha. Nne, ijadiliwe rasimu ya Waryoba na si ya CCMM wala nini. Tano, wale wote wanaopinga rasimu ya Waryoba wawekwe ndani kwanza na kuachiwa baada ya kuandikwa katiba mpya.”
Kabla ya kuendelea Kanji anakwanyua mic, “Somi nakosea sana. Kwanini funga vatu kwa kutoa wazo yao?”
“Wangekuwa wanatoa mawazo yao na kuacha hujuma kusingekuwa na haja ya kuwafunga. Angalia wanavyopoteza muda na njuluku zetu kutetea uoza wao. Hii haitakubalika hata kidogo.”
Mijjinga ang’aka, “Lazima wafungwe hawa wapuuzi. Pia hawa matapeli wa kinigeria wanaotoa tuzo za kipuuzi waonywe.” Anafungua mkoba wake na kutoa kijikaratasi chenye anwani mojawapo ya matapeli wa Kinigeria. Anasema, “Tuwaandikie barua ya karipio.” Anakunjua kijikaratasi na kusoma anwani ya hawa matapeli kwa sauti akisema, “Ofisi zao za kishenzi zipo Namba 13 Mambilla street, Off Aso Drive, Asokoro.P. O. box 9824, Garki, Abuja, Nigeria.” Anashangiliwa kwa utafiti wake uliokwenda shule.
Baada ya hapo kijiwe kinakubaliana kuandamana hadi ofisi za Wizara ya Sheria na Katiba na Uhamiaji kuwatimua manyang’au.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 13, 2014.

3 comments:

Anonymous said...

watanzania tu wabumbavu sana tena wajinga wa kufikiri wala kuwaza
ndo maana CCM wanatuchezea kwa masilahi yao
MWENYE UCHUNGU NA TANZANIA HAWEZI KUWA CCM WOTE LAO MOJA

Anonymous said...

watanzania tu wabumbavu sana tena wajinga wa kufikiri wala kuwaza
ndo maana CCM wanatuchezea kwa masilahi yao
MWENYE UCHUNGU NA TANZANIA HAWEZI KUWA CCM WOTE LAO MOJA

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umenena ila kuhukumu watanzania wote si sawa. Wapo wapumbavu kweli kama hao uliowataja na chama chao. Je sie tusikuwako huko nasi unatuweka kwenye jungu moja?