How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 5 March 2014

Kijiwe chstukia EPA mpya

SIKU hizi kijiwe kimegeuka FBI ya kaya. Kila inapotokea skandali lazima mmoja wetu awepo.
Leo ni zamu ya Mijjinga al maarufu Shed. Anaingia akiwa na makabrasha yake huku akiwa ameniga bonge la tai.
Anaamkia kama kawaida yake huku akitoa mkono karibu kwa kila mmoja wetu kabla ya kukaa kwenye nafasi yake karibu na deli la kahawa.
Kabla hata hajasema lolote, Mpemba anamtania. “Yakhe leo watakaenda Dodoma kujiunga na Mgosi Machungi na walaji wengine ili mtetee kuongezewa ulaji hata kabla hamjafanya lolote?”
Mijjinga naye anaamua kumjibu kwa kuigiza lafudhi ya Kipemba akisema: “Yakhe wala huko sendi. Mie si kama wale wapendao kula bila hata toa jasho wallahi.” Kila mmoja anaangua kicheko jinsi alivyopatia lafudhi ya Kipemba.
 Anamgeukia muuza kahawa wetu aitwaye Shem na kusema, “Bwana Shem hebu kwanza nifanzie kitu lau nilainishe koo ili nijenge kesi yangu niliyoleta hapa kijiweni.”
Akiwa anatabasamu, Shem hajibu kitu bali kumwekea kahawa na kuweka mbele yake kwenye meza.
Mijjinga anaibwia kahawa kama funda tatu nne na kuanza, “Waheshimiwa, kaya hii kweli imeingiliwa sijui tutaiokoaje ndugu zanguni?”
“Wewe!” Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu anachomekea na kuendelea, “Matusi sasa. Yaani wewe ni wa kusema kuwa kaya nzima imeingiliwa?”
Kabla ya Mijjinga kujibu, Mipawa anakula mic, “Tatizo lenu ni kubadili maana ya kila jambo. Kama wewe huoni kaya ilivyoingiliwa basi una matatizo.
Hivi huoni wageni wanavyojiingilia tena wakiwa wahamiaji haramu na kuua hata tembo wetu na kufanya kila aina ya jinai na kujiondokea na utajiri wetu?
“Nami nasema kaya imeingiliwa kuanzia juu hadi chini na wanaoongoza kwa kuingiliwa huku ni watawala wetu ambao wametelekeza majukumu yao na kujiingiza kwenye ujangili na ujambazi.” Anapigilia msumari Kapende huku akimuangalia Mijjinga kana kwamba walipanga muvu hii.
Mijjinga anaendelea, “Nitatoa ushahidi ndugu zanguni kuonyesha watawala wetu walivyoingiliwa na mdudu mbaya wa upogo upofu na tamaa.”
Anafungua mkoba wake na kutoa gazeti la Waambie Kavu Kavu lililoandika, “Mkaguzi Mkuu wa Pesa za Serikali (MM-PESA) bwana Lud Uto, amegundua wizi wa zaidi ya dola milioni 300 kwenye Hazina kuu huku akikosa maelezo juu ya upotevu huu hata alipowasiliana na waziri wa Njuluku Saaada Mkuyati.”
Kabla ya kuendelea, mzee Maneno anachomekea, “Hii HEPA nyingine wajameni.”
Msomi aliyekuwa akiangalia na kutikisa kichwa anaamua kutia guu ili kumwaga lecture. Anabwia tangawizi yake na kukohoa kidogo na kumwaga sumu. Anasema, “Kinachogomba kwangu si wizi tu.
Wakati umma wa makapuku ukiibiwa matrilioni kama haya wale wanaojiita wawakilishi wao wako bize wakimalizana wakigombea laki tatu za Katiba Mpya wakati wakiacha wezi wajizolee dola 300,000,000 ambazo ni sawa na trilioni zaidi ya 45 kwa njuluku za madafu.”
Kabla ya kuendelea, mzee Mdomo anauliza, “Hivi trilioni ina masifuri mangapi?”
“Siyo trilioni ni trilioni.” Anakosoa Mipawa ambaye muda mwingi alikuwa akisoma lile gazeti na kuapa na kutukana matusi mazito ya nguoni akitishia kumnyotoa mtu roho hasa wale walioiba haya matrilioni.
Msomi anaendelea kudema, “Nashangaa hawa wasasi wa ngawira wanaojiita wawakilishi wetu. Sijui hawasomi magazeti. Maana hii HEPA ni mama wa EPA kwani ile ya kwanza ilikuwa chini ya nusu ya hii.”
Kabla ya kuendelea Mpemba anauliza, “Hivi ile EPAA ilikuwa kiasi gani?”
Mbwa Mwitu anamuonya, “Ami sauti hiyo. Kaza noti yasiwe yale ya Popobawa.”
Msomi anaendelea; “Wachovu kwa kusahau sijui mmeingiliwa na nini! Yaani hata EPA ya juzi tu umeishaisahau!”
Kabla ya kuendelea Kanji anakula mic, “Vatu hapana soma gazeti dugu yangu Somi. Kama soma hapana iko kumbuka. Mimi ona gazeti nyingi fungia tumbua na ndazi.”
Bi Sofia Lion aka Kunungaembe anatia guu kama kawaida yake. Anasema, “Heri sie huku twafungia magazeti maandazi kwa vile tu wastaarabu, pale nchi jirani wayatumia kuchambia.”
“Hata Bombai mimi ona gazeti chambia na sikini jengea jumba,” Kanji anamuunga mkono mshikaji wake Sofi Kanungaembe a.k.a Open Check.
Msomi anaendelea, “Hii EPA iliyoripotiwa ingawa umma umeinyamazia bila shaka inalenga kufanikisha uchakachuaji.
Maana ukiangalia hata ile EPA ya kwanza ya mwaka 2005 iliasisiwa na na kutekelezwa na Ben Makapu Tunituni akimsaidia kibonde wake Njaa Kaya ili baadaye amlinde kwa kutumia rungu la urahisi ilifanyika karibu na uchakachuaji.
Hivyo, mimi sishangai hasa usawa huu ambapo vibonde na vidokozi kama Muigulu Michembe na Adum Milima walipelekewa kule chini ya kihiyo Saaada Mkuyati.”
“Du Beng’we natamani nile nyama ya fisadi ndugu zanguni. Hii EPA nyingine na mshiko unapelekwa Jersey na Uswisi wangu wangu!” Anachomekea Mipawa kwa hasira.
Msomi anaendelea, “Kwa taarifa yenu hadi unafika wakati wa kuchakachuliwa na kutapeliwa tena kwa ahadi tamu tamu na nyingi, lazima sarafu yenu ya madafu ishuke kama vile inaharisha.
Kwa lugha ya kitaalamu ya Kisukuma hii huitwa double digit inflation. Mara nyingi hii hutokea kila baada ya uchafuzi aka uchaguzi aka uchakachuaji. Unaweza kuangalia trajectory ya sarafu yenu ambayo siku zote huporomoka kama inaharisha kuanzia siku alipoachia ngazi gwiji Mchonga hapo mwaka 1985, 1995, 2005 na sasa 2015.”
“You are dead right Doctor Msomi,”Nami naamua kukatua mic na kutoa mchango wangu.
Msomi ambaye leo amekuwa msemaji mkuu anasema, “Usemayo ni kweli profesa Mpayukaji. Sisi magwiji wa uchumi tunayajua haya japo wahusika wanajifanya kutotusikiliza.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si Mgosi Machungi alimpigia simu Msomi akitaka atupe salamu toka Mjengoni.
Kila mmoja alikuwa bize kugombea kisimu cha Msomi ili angalau azoze na Mgosi anayesema kuwa yeye na bi mkubwa wake yaani Mama Abdallah wameishachukua mshiko na wako zao Tuliani wakijituliza na kutuliza.
Tukiwa hatuna hili wala lile si gari la Saaada Mkuyati likapita, kwa hasira tuliamua kulimwagia kahawa tukizomea EPA EPA EPA hadi dereva akahepa kama wezi wa EPA na HEPA nusu agonge wapita njia!
Chanzo: Tanzania Daima Machi 5, 2014.

2 comments:

Jaribu said...

Kijiwe kishachelewa. EPA nyingine ishafanyika. Kama kawaida "Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Mataifa Ya Uwekezaji ya Washington DC, iliamua hela zilizokuwa zinaibiwa TANESCO za dola laki mbili kwa siku ziwekwe kwenye escrow accounts mpaka Saada Taahira, I mean Mkuya atakapochaguliwa. Mbona miaka yote Marekani sijaisikia hii "Mahakama"?.

Halafu huyu Mjinga Rugamarila anasema hizo ni vijipesa vya ugoro. Hela za kuchakachua zishapatikana hapa. Huyo Rugawhatever ni kuwadi tu, Dakta ndiye anaendesha usukani.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

IPTL haikutushangaza kwa vile iliundwa wakati Dr Zero akiwa waziri wa wizara husika. Huyu Rugefirira sijui Rugemalira kama usemavyo ni pawn wa kawaida anayetumiwa na mabwana zake akina Dr Zero na Benjamin Mkapu Tunituni. Hata hivyo wacha waibe maana waibiwao nao wako kimya wakitamani wangekuwa wao nao wahomole si unaijua Bongo yenu.