The Chant of Savant

Wednesday 16 May 2012

Barua ya wazi kwa waziri wa elimu

Ndugu waziri, Dk. Shukuru J. Kawambwa.
Kwanza, naomba nisikuite mheshimiwa. Sina haja ya kueleza ni kwa nini.
Naamini unajua kuwa uheshimiwa wa siku hizi si chochote si lolote bali wizi wa mchana. Watu wenyewe wanaoitwa waheshimiwa hawastahiki hata chembe ya heshima. Hayo tuyaache.
Hivyo, nisamehe sana kwa kukunyima ukuu huu ambao, kwa hali ilivyo, huustahili hata chembe. Utastahilije ukuu wakati elimu yetu haina heshima wala maana tena? Itapata heshima wapi iwapo watoto wetu wanamaliza shule za msingi hata sekondari bila kujua kusoma na kuandika lakini tunafungwa kamba kuwa wameshinda.
Wameshinda kweli au wameshinda katika kuongeza ujinga? Ila wakati hayo yakiendelea, watoto wenu mnasomesha nje tena kwa kodi za haohao mnaowajaza ujinga.
Bwana waziri, nakupongeza kwa kubakizwa kwenye nafasi yako ingawa hakuna ulilofanya la maana kustahili kubakia. Nani ajua? Au ni yale ya zimwi likujualo mwanakwetu?
Mwaka 2008 ulipoteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na makando kando yake nilifurahi nikiamini ungeondoa madudu yaliyofanywa na Profosa Jumanne Maghembe ambaye legacy aliyoacha ni kuizika elimu ya Tanzania. Kumbe nilikuwa nimekosea. nilidhani kama mwanataaluma aidha ungeboresha shule za kata au hata kuzifutilia mbali maana ni mazalio ya ujinga kutokana kutopewa zana, walimu hata sera za kitaaluma.
Zimekuwa shule za kisiasa ambazo hutumiwa na wanasiasa wachovu kujisifu kuwa wameongeza idadi ya shule wakati ni upuuzi mtupu.
Kilichonisukuma kuandika waraka huu si kingine bali kukutaarifu kwa ukweli bila woga kuwa mmeua elimu kutokana na sababu mnazojua wenyewe mojawapo ikiwa ni kuandaa mazingira mazuri kwa watoto wenu mnaowasomesha nje kwenye shule za maana ili nao baadaye wawatawale wajinga wetu mliowajaza ujinga nyongeza kwa waliokuwa nao.
Ingawa hii ni visheni yenu, mfahamu kuwa kutawala wajinga ni kazi hata kama kutawala wasomi kuna changamoto nyingi. Watoto wenu mnasomesha Ulaya na Marekani huku wale wa walalahoi mkiwakalisha kwenye mawe kama nyani ukiachia mbali kuzidi kuiharibu elimu hata kiwango kidogo tulichoachiwa na Mwalimu Nyerere.
Kwa wanaokwenda vyuo vya juu ambavyo navyo havina hadhi tena kama zama zile, mnawasulubu na mikopo wakati nyinyi mlisoma bure.
Leo nchi yetu imejaa International schools na academia ambazo si International wala Academia kitu bali utapeli mtupu. Hata kama kuna baadhi za kweli, kwa mamilioni ya shilingi wanayotoza ni Watanzania wangapi wataweza kupeleka watoto wao kule?
Kwa nini hamkumbuki ukweli kuwa nyinyi ni watoto wa makapuku waliosoma bure chini ya siasa mnayokandia ya Ujamaa na Kujitegemea ya Mwalimu Nyerere? Hivi Nyerere angekuwa mchoyo kama ninyi wengi mngekuwa wapi kama siyo kuwa sawa na hawa tunaoona wakichomwa moto kwa vile hawakupata fursa ya kuelimika?
Ndugu waziri, hata kama wewe si ndugu, hakuna kitu kinanikera na kunichefua kama kuona wengi wa Watanzania wanavyopeleka watoto wao nchi jirani kama Kenya na Uganda. Nasikia hata siku hizi wengine wanapeleka hata Rwanda!
Ingawa wewe huwezi kupeleka watoto wako kule ukweli ni kwamba wengi wanadhalilishwa hata kutapeliwa kutokana na kuandikishwa kwenye shule zisizo na viwango wala maadili bali madili. Hivi ulishajiuliza kama binti au mwanao angekuwa kule akitaabika kiasi cha wengine hata kuanza kuwekana kinyumba ili kumudu gharama za maisha?
Hakuna kitu kilinitisha kama kile kilichofanywa chini ya mwenzio aliyekutangulia aitwaye Majembe sijui Mapanga. Nilipoangalia mitaala nilitaka kufa kwa ugonjwa wa moyo kutokana na jinsi ilivyovurugwa na kuongezwa ujinga badala ya taaluma.
Nasikia, kwa mfano, vitabu vya fasihi na sanaa hivisomwi tena. Kama ni kweli kuwa wanafunzi wanasoma kitabu kimoja badala ya vingi ili kujifunza kufikiri na kupambanua mambo, basi kuna siku watu watakojolea makaburi yenu na kutamani mgekuwa hai ili wawaadhibu kama wawafanyavyo vibaka.
Juzi nilikuwa naongea na mchapishaji wangu aliyeniambia kuwa wachapishaji sasa wanafunga ofisi zao kutokana na kutokuwa na soko la vitabu vya kiada. Ajabu wakati madudu haya yakiendelea bado mnajisifu kuwa mmepanua sekta ya elimu wakati ukweli ni kwamba mmeishaiua na mnachofanya sasa ni kuizika. Je mnataka tuwe tunanunua vitabu vya kiada toka nje?
Ingawa hamtaki kuona mbali, msishangae siku moja mkinunua Kenya. Juzi nilishtuka nusu ya kukata roho baada ya kugundua kuwa hata Kiswahili kinachotumika kwenye mtandao kama lugha rasmi ni cha Kenya na si cha Tanzania.
Siku hizi Kiswahili kwao Kenya siyo Tanzania tena toka na ufisadi huu wa kielimu. Je, kuna upogo kama huu duniani tena unaofanywa na taifa kutokana na kikundi kidogo cha watu wabinafsi na waroho wasioona mbele?
Mmeua hata watunzi na wachapishaji kienyeji hivi hivi! Au mnaridhika na wanafunzi kusoma udaku ili hapo baadaye wawe wadaku badala ya wasomi ili watoto wenu watawale kimteremko?
Leo sisemi mengi ila mnatia aibu kuna kesho mwaweza kulipia kwa njia ambayo hamkutarajia. Kuna haja ya kufikiri kwa kuangalia wakati ujao badala ya kuangalia usawa wa pua.
Kila la heri. Tafakari mapema kuna kesho. Hivyo, kuna haja ya kusoma alama za nyakati kama mwanataaluma na mwananchi anayeamini kuwa kila kitu kina mwisho.
Je, utajisikiaje miaka 20 ijayo utakapogundua kuwa wajukuu zako wanasoma kwenye shule zinazowajaza ujinga kama ilivyo sasa?

No comments: