Gazeti la kila siku la Kiswahili la
Mwananchi Jumatatu 9 Aprili mwaka huu lilinistua sana kutokana na kichwa cha
habari lilichobeba siku hiyo. Kichwa chenyewe kilisomeka, “Mwanzo, mwisho wa
Steven Kanumba, JK aahirisha safari ya ughaibuni kumlilia, kuzikwa
kesho.”
Kutokana na kuishi mbali na kutokuwa
shabiki wa filamu hasa za kisasa zilizojaa matusi na mambo ya mapenzi tu, ni
bahati mbaya kuwa sikumjua Kanumba. Hii ikichangiwa na kutozipenda
sanaa za Tanzania hasa muziki ambapo wasanii huimba mapenzi kuanzia asubuhi hadi
asubuhi, ni bahati mbaya sana kuwa siwajui wasanii wetu wengi hata kama
wanajulikana. Ukiongeza na ukweli kuwa Kanumba alianza kujulikana baada ya mimi
kuondoka Tanzania ndiyo basi.
Katika kichwa cha habari tajwa hakuna
kitu kilinishangaza kama kusoma kuwa rais Jakaya Kikwete aliahirisha safari ya
ughaibuni si kwa kuogopa kuwaongezea mzigo watanzania kutokana na tabia yake ya
kupenda kusafiri bali kumlilia Kanumba, nilishangaa na kuanza kujiuliza huyu
Kanumba ni nani ambaye umuhimu wake ni mkubwa hivi kiasi cha kuvunja rekodi ya
Kikwete katika utendaji wake? Nilijiuliza swali hili kutokana alichofanya wakati
wa mgomo wa madaktari ambapo hakuahirisha safari yake kwenda kwenye mkutano
ambao hakukuwa muhimu sana kule Davos.
“Nimeguswa na msiba huu, nilikuwa
nisafiri lakini nimeamua kuja hapa kuwapa pole ndugu na wasanii wote,”
alikaririwa akisema Kikwete. Kumbe Tanzania watu wanazidiana!
Kikwete hakuguswa na vifo vya watanzania wakati wa mgomo lakini
aliguswa na kifo cha Kanumba. Wasanii wanasifika kwa rais Kikwete kuliko
madaktari na wengine? Acha aitwe msanii huenda ni msanii mwenzao. Ama kweli
waarabu wa Pemba hujuana kwa vilemba! Huku ndiko kufanya mambo ya
hovyo muhimu na ya muhimu hovyo kama tutatangalia ukweli. Niliwahi kulalamikia
tabia ya watanzania kuwekeza katika glosari na nyumba za kulala wageni huku
wakenya wakiwekeza kwenye viwanda na waganda kwenye kujenga mashule. Hii maana
yake ni kwamba tukiungana afrika mashariki, ukitaka maraha utayapata Tanzania.
Ukitaka biashara utakwenda Kenya na ukitaka elimu bila shaka
Uganda.
Je ni kwanini wasanii ni bora kuliko
madaktari? Jibu liko wazi kuwa wanaburudisha na hii ni nchi ya burudani. Ukitaka
kujua nimaanishacho, nenda kituo cha polisi kuomba ruhusu ya kucheza ngoma wiki
nzima hata kwa kufunga mtaa utapewa. Lakini ukienda kuomba kibali cha kuandamana
kupinga uongozi wa kifisadi wa mtaa utawekwa ndani bila shaka. Hii ndiyo
Tanzania ya sanaa na maraha. Hata ukiangalia miziki yetu, huongelea burudani
hasa mapenzi. Kama wapo wanaoongelea maisha ni wachache sana ukilinganisha na
majirani zetu. Hebu sikiliza miziki inayochezwa kwenye vituo vyetu vya radio
hata runinga, ni mapenzi, mikasi, matusi na upuuzi mwingine. Zama za miziki
inayohimiza kilimo, kuamka mapema kwenda kazini na kusoma kwa bidii ishapitwa na
wakati. Hata watawala waliohimiza wananchi kufanya kazi kwa nguvu na
kujiendeleza walishapitwa na wakati. Tuna watawala wanaokwenda sambamba na
wasanii hasa wanaowatumia kwenye kila kampeni zao za ulaji.
Ingawa kitendo cha rais Jakaya Kikwete
kukaririwa akisema kuwa aliahirisha ziara ili kumuomboleza na kumzika Stephen
Kanumba kinaweza kuonekana ni cha utu, ukweli ni kwamba kinaacha maswali mengi.
Wengi tunajiuliza: Kanumba ni bora kuliko watanzania waliopoteza maisha wakati
wa mgomo wa madaktari uliosababishwa na uzembe wa Kikwete?
Je Kikwete amefanya hivyo kwa dhati au
kutafuta tukio la kufunika aibu iliyokipata chama chake kushindwa kule Arumeru
Mashariki? Je Kikwete ana uchungu na msanii mwenzake kuliko watanzania wenzake?
Kikwete alinukuriwa na magazeti akisema, "Nimeguswa na msiba huu, nilikuwa
nisafiri lakini nimeamua kuja kuwapa pole ndugu na wasanii wote," Wenye
kumbukumbu wanajiuliza: Mbona hakufanya hivyo wakati wa mgomo? Mbona hakuguswa
na misiba ya watanzania wakati wa mgomo alipoamua kuwaacha wakilia akaekea zake
Davos Uswisi kwenye mkutano ambao hakuwa na umuhimu?
Laiti Kikwete angeahirisha safari yake
kwa kuguswa na vifo vya watanzania wakati wa mgomo, angejizolea sifa na heshima
kubwa. Maswali yanaendelea. Je ni kutafuta sifa rahisi rahisi au
kutaka kujionyesha kama mpenda watu? Je lipi bora, umahiri wa kuhudhuria mazishi
na misiba au kutatua kero za wananchi? Washauri wa Kikwete wanapaswa kurejea
darasani kujifunza upya. Wafanye hivyo haraka ili kurejesha heshima ya taasisi
ya urais bila kujali kuwa anayewashauri kufanya hivyo ni Nkwazi Mhango au nani.
Msiangalie majina yetu bali tunayowaambia ili kuepusha aibu inayoendelea
kuikumba taasisi ya urais kiasi cha kuanza kuonekana kama taasisi ya urahisi na
si urais.
Ingawa ni haki ya rais kumuombolezea
ampendaye, anafanya kufanya hivyo kwa kuangalia mantiki ya kufanya hivyo
akionyesha hadhi ya cheo chake. Vinginevyo hata kwenye msiba tajwa angeweza
kumtuma waziri husika lakini siyo kujifungasha yeye, mkewe, waziri mkuu, makamu
wa rais na wengine wengi bila sababu. Kama hakuna namna au tuseme
kukwepa aibu ya kichapo cha Arumeru Mashariki, mbona hatukuona umuhimu kama huo kwenye mazishi ya aliyekuwa shujaa wa vita ya Kagera na mkuu wa majeshi marehemu
General Mwita Kiaro?
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 18, 2012.
|
How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday 18 April 2012
Kikwete, wasanii, madaktari na usanii
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment