Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Wednesday 4 April 2012

Poleni watu wa Mtera kwa kuanguka mikononi mwa chizi

 
Mbunge wa Mtera CCM, Livingstone Lusinde aka Kichaa akirapu rapu zake za matusi  ya nguoni kule Arumeru Mashariki hivi karibuni.

KAMPENI zilizopita za uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, zilifichua mambo mengi hasa uhovyo wa siasa na viongozi wetu. Mambo yalianza na wazee wazima Benjamin Mkapa, rais mstaafu, kujivua nguo kwa kujifanya msemaji wa ukoo wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alimtengeneza na kumnadi Mkapa lakini baadaye akamwangusha vibaya kiasi cha kufa akiwa analilia Watanzania wake.

Nani mara hii kasahau maneno ya mke wa marehemu, Mama Maria Nyerere aliyesema kuwa maneno ya mwisho ya mumewe yalikuwa, "Nawalilia Watanzania wangu"?

Hii maana yake Mwalimu alikufa na roho iliyojikunja; ikizingatiwa Watanzania aliokuwa akiwalilia walikuwa kwenye mikono ya mtu wake lakini aliyeonyesha wazi kuwa wa hovyo kisera.

Mwingine aliyejivua nguo ni mzee Stephen Wassira, Waziri wa Uhusiano na Uratibu Ofisi ya Rais ambaye alianzisha ligi ya matusi na uongo kwenye kampeni kiasi cha kugeuka kuwa uwanja wa wahuni wa chama chake kuja kuonyesha uhuni na uhovyo wao. Wassiara alikaririwa akimtuhumu katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kula pesa ya maandalizi ya ujio wa Papa John Paul II mwaka 1990, madai ambayo yalipingwa vikali na Kanisa Katoliki ambalo bosi wake ndiye alikuwa akitembelea Tanzania.

Rais wa TEC, Askofu Mkuu Juda Thaddeus Ruwa'ichi alimjibu Wassira kwa maneno haya, “Ukiona mwanasiasa anakurupuka na kuanza kumchafua mwenzake ujue amefilisika, vitendo hivyo vinaonyesha udhaifu kwa nchi katika nyanja za siasa,”

Hayo ya Mkapa na Wassira yalikuwa cha mtoto au tuseme ufunguzi tu. Maana baba yao katika ligi hii ya matusi, Mbunge Livingstone Lusinde wa Mtera (CCM) alikuwa hajaja kumaliza kazi hii aliyotumwa na chama chake. Alikaririwa akitamka maneno ambayo si vizuri kuyarudia na wala hayafanani na mtu wa umri na wadhifa wake kama mbunge mwakilishi wa wananchi. Hivi mtu anayeweza kusimama kwenye jukwaa la siasa kutangaza sera akatangaza matusi tena kwa kuiga maneno ya vikundi vya maigizo, umuweke kundi gani? Zamani wengi tulikuwa tukikwazwa na salamu za Mkapa za kihuni za “MAMBO” bila kujua kuwa kumbe kuna wahuni zaidi.

Lusinde alikaririwa akisema kuwa kama CHADEMA ni vichaa wa kurogwa basi yeye ni wa kuzaliwa. Ni bahati mbaya na hasara kuwa na viongozi aina ya Lusinde. Je, ilikuwaje watu wa Mtera wakamchagua chizi anayekiri kuwa chizi tena tangu kuzaliwa? Je, alipitaje kwenye mchujo au ni yale yale ya wananchi kuchoka utawala wa mtu mmoja na wa kurithishana kutokana na ukweli kuwa mbunge wao wa zamani John Malecela alikuwa amewachosha kwa kukaa madarakani kwa muda mrefu?

Nashindwa kujua mantiki ya kumchagua mtu wa hovyo na kichaa kama huyu anayeweza kusimama jukwaani na kuwadhalilisha wenzake tena mbele ya watoto wadogo akionyesha uhodari wa kuchambua mavazi ya wenzake badala ya matatizo ya anaowawakilisha?
Hivi mbunge anaposimama jukwaani na kugeuza mdomo wake sehemu ya kutolea uchafu, tena mbele ya kadamnasi na watoto, anajenga picha gani? Je, huu si ushahidi tosha kuwa CCM imeishiwa kiasi cha kushabikia uhuni na mipasho ya kipumbavu? Je hii si kuigeuza CCM kuwa Chama Cha Matusi? Hata waimbaji wa taarabu za matusi na hata rap wana afadhali kwa vile wayafanyayo ni saizi yao.

Sijui kama Lusinde anasoma hata magazeti zaidi ya yale ya udaku kama alivyothibitisha kwa kauli zake za kichovu na kiwendawazimu. Je, maneno na tabia vya Lusinde vinakisaidiaje chama chake zaidi ya kukibomoa? Maana ukiangalia kuzodolewa, kwa mfano, kwa Wassira hata Mkapa ni ushahidi tosha kuwa CCM iko pabaya na imeishiwa.

Je yote haya ni matokeo ya kuua maadili na kuingiza madili kwenye nafasi yake? Maana kwa nchi yenye kufuata sheria na kanuni za maadili, tume ya uchaguzi (NEC) ilipaswa kutoa tamko hata karipio mara moja Lusinde alipogeuza kampeni uwanja wa kushindanisha ukichaa na matusi ya nguoni.

Hivi mtu anayeweza kuwaita wanaume wenzake mashoga na wajawazito ana akili kweli? Heri angeishia pale. Wenye mtindio wa akili wenzake wangedhani amewajibu wapinzani japo siyo. Nani mara hii alivyowaambia wapiga kura kuwa yeyote ambaye hataichagua CCM ni mjamzito? Je, ujauzito ni ugonjwa? Hivi bila ujauzito mama yake angemzaa kweli? Je kutukana watu kwa kutumia ujauzito si kuwadhalilisha wanawake na mama yake akiwamo? Maana huo ujauzito usio na baba maana yake ni umalaya.

Maneno ya Lusinde ni ushahidi kuwa hakupata malezi mema wala elimu ya kutosha kiasi cha kujenga taswira kuwa huenda alizaliwa mitaani. Maana hata tofauti na wahuni wanaopiga debe kwenye mabasi ya daladala wala wauza mitumba Mtaa wa Kongo. Heri ya wao wamefukarishwa na akina Lusinde kuliko Lusinde anayelipwa kodi ya wananchi kwa kuchafua maadili akilinda na kutetea uozo na mgando wa mawazo. Tena uoza wenyewe utawala wa kurithishana kama walivyoonyesha kwenye kuteua wabunge wa Jumuia ya Afrika Mashariki!

Kama siyo CHADEMA kuchelea kukimbizana na kichaa, ilifaa afunguliwe mashitaka. Hata hivyo, kwa kauli za watajwa watatu, kama CHADEMA watashindwa basi wana kila sababu ya kwenda mahakamani na kudai uchaguzi haukuwa huru na wa haki. Maana haki na uhuru ni heshima na si kashfa tena za kuzua na matusi. Laiti Lusinde angewatuhumu CHADEMA mambo ya kweli, hakuna ambaye angehangaika naye. Litakuwa jambo la ajabu na hatari kama CCM na Tume ya Uchaguzi hawatamchukulia hatua za kinidhamu tena za wazi Lusinde.

Kuna haja ya wachambuzi wa mambo kudodosa na kupata historia ya Lusinde ili apewe msaada na wale waliofanya kosa kumwamini wadhifa wa heshima kama ubunge. Kimsingi lugha na matusi ya Lusinde yamewadhalilisha wabunge wote hasa wa chama chake na uongozi mzima. Hivi kama Lusinde ana mke na watoto hata wazazi wake sijui amewaumiza kiasi gani kwa kujivua nguo hadharani hivyo? Poleni sana watu wa Mtera. Huenda ni yale yale kuwa atukanaye wakubwa haishii na mmoja.

Alimtukana John Malecela akazoea sasa anataka kumtukana kila apitaye. Si ajabu akitofautiana hata na mwenyekiti wake hatakosa kumfurumshia mitusi ya nguoni kama alivyozoeshwa na chama chake. Poleni wapiga kura wa Mtera kwa kudhalilishwa na Lusinde ambaye aliwakilisha matusi badala ya heshima na matatizo yenu.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 4, 2012.

No comments: