The Chant of Savant

Wednesday 11 April 2012

Mzoga wa bei mbaya na mafisi wauza fisi


BAADA ya kurejea kutoka kwenye dhambi, kitambo, kama miezi sita hivi sikupata ndoto wala ufunuo. Baada ya kumrejea wadudi si haba. Naona mambo yanaanza kunyoka kiasi cha ndoto na unabii kurejea kama kawa.
Niliwahi kuwataarifu nilivyooteshwa dawa ya kupambana na matatizo mbali mbali kama mgawo wa umeme ambao umepungua, kuporomoka kwa madafu yetu yaitwayo pesa, kuanguka anguka kwa wazito ambao sasa wanaonekana kutakata na mengine mengi, Wangekuwa wangonjwa wa miwaya tungesema wanatumia EIARAVII. Hata hivyo, nani anajua?
Kwanza, inapaswa nionye. Mie sijaoteshwa upuuzi kama yule tapeli wa Loliyondo au matapeli wengine wanaohubiri kutenda miujiza wakati ni utapeli na ujambazi mtupu. Hivi ni mpuuzi gani huyu anayewapa vibali vya kutenda jinai tena kwa kaya nzima? je huyu si mgonjwa wa kuwekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi?
Ndiyo nimeamka. Nimefunuliwa ambayo hayajawahi kufunuliwa kwa yeyote. Naona watu wenye njaa na wagonjwa wakigombea kununua mzoga unaonuka! Mzoga wenyewe unauzwa bei mbaya. Wajua ni bei gani? Elfu hamsini na ushei za madafu! “Sadakta toba Mola tusitiri!” Mmojawapo asiye mlevi anajisemea.
Huu ni ukichaa au ujuha yarabi? Nawaza rohoni. Wangejua mzoga wenyewe kibudu tena wa mnyama haramu-fisi, wasingehamanika. Ajabu walliaahidiwa kondoo na mbuzi na kuku wakaishia kuletewa mbwa! Hata hivyo, adui yako muombee njaa. Njaa inapopanda kichwani huwa balaa. Heri njaa ya tumbo kuliko ya kichwani.
Watu walivyokuwa wamehamanika, nilikumbuka juzi nilipokuwa Arushameru nikishuhudia vichaa kama Lushinde wakitukana watu wazi wazi kabla ya vichaa wengine kama vile Denjaman Makapi na Stivi Wahasira kuja na kufanya ukichaa wao.
Nilikumbuka watu walivyokuwa wakihamanika kuwasikiliza vichaa hawa sawa na hawa niliowaona ndotoni wakigombea kununua nyama ya fisi. Hakuna siku nilitaka kufa kwa mshtuko kutokana na kumuona Ewassa yule kinara wa mafisadi naye akitia timu Arushameru kumpigia kampeni Mkazamwana eti.
Hayo ya vichaa ambao hayana tofauti na mzoga maana unapoanza utawala wa kisultani wa kurithishana huna tofauti na kula mzoga tena kibudu. hata hivyo, nashukuru Mungu watu wa Arushameru walikataa usultani na utawala wa kikuli wa matusi ya nguoni wizi na ujambazi wa mchana.
Turejee kwenye mzoga wa bei mbaya. Ili kuwazuzua na kuwashawishi walevi na majuha, wauza fisi walimpaka mafuta akanawiri halafu wakafungia kichwa na miguu yake kwenye gunia huku wakionyeshwa mbavu wasijue fisi!
Wachuuza mbwa hawa walisikika wakiwaambia walevi: “Tunawaleta MM yaani Mbuzi Mkubwa au mlo mlo,” wasijue siyo!
Nao kwa uroho na imani haba inayoweza kuamini kila miungu wakauingia mkenge kichwa kichwa huku wakichangishana ili kununua mbwa wapate nyama na kufaidi wasijue watafaidiwa wao baada ya kutapeliwa!
Mtabiri mmoja mwenye akili aliwaonya walevi na majuha kwa kuwaambiwa kwa kifupi akisema: “Mnauziwa JeiKei, yaani Jifisi Kubwa siyo MM yaani Mbuzi Mkubwa.” Nilisikia kijana mmoja wa kihuni akimwambia mwenzake kwa mafumbo.
Alinikumbusha zama zile za wapambe walipowadanganya wadanganyika kuwa kilaza fulani aweza kuwakomboa wakati yeye ahitaji ukombozi. Maskini majuha hayakustuka zaidi ya kuzidi kuchangishana njuluku yasijue yanamchangia mbwa na muuza fisi!
Ajabu wanadi nyama ya fisi, kwa ufisi na ufisadi wao, walizunguka kijiji kizima huku na huko wakikusanya pesa ya kununua nyama ya fisi bila kustukiwa huku fisi aliyefungwa kwenye gunia akipandishwa kila meza ili watu waone mmeto wake! Je, hapa tatizo la watu hawa wa ndotoni ni ujuha, uroho, upofu, upogo au hamnazo?
Jamani mshaambiwa mnachogombea si kitoweo bali nyama ya fisi. Je, mnataka tuwasaidieje mjue mnaliwa tena kwa kulishwa haramu tupu? Shauri yao kama hawataki kuelewa acha wateketee.
Juzi hamkuwasikia kunguru wakianza kuraruana wakigombea mzoga wao? Inakuwa hatari waja wanapogeuka kunguru au kufanana nao.
Najua wasomaji wengi wanajiuliza. “Huyu mbona naye kazibuka na kutufumba.” Sifumbi. kila mtu ana jibu na anaweza kuona ukweli kama ataamua kuutafuta. Tumia akili. Siku zote ndoto zina watafsiri wake.
Kimsingi, ndoto yangu inaweza kutumika kwenye hali yoyote ambapo watu wasio na hatia hufanyiwa vitu haramu wakavihalalisha badala ya kuviteketeza na hao waviletao kama ilivyo kila mahali karibu katika kila kitu. Je mnataka nifumbue zaidi ya hapa? Never. Nanyi tumieni akili yenu japo kidogo.
Quod ubique, quod semper, quod omnibus walijisemea walatini. Tafsiri ni kwamba kinachoabudiwa na wote wakati wote na kila mahali. Kwa Danganyika linapokuja suala la ulaji, ni ibada mtindo mmoja.
Hata wale waliokuwa wamejificha nyuma ya majoho nao wameingia kwenye ibada hizi za sanamu na vipande thelathini vya fedha! Namna hii tutanusurika kweli? Hamjayasikia mafisi yaliyovaa ngozi za kondoo yakiwakingia kifua chui yakidhani hatujui?
Ngoja nifumbue kidogo. Hivi mtu anayekupa ahadi za kitoto na kipumbavu asitekeleze hata moja siyo muuza fisi? Je yule anayekudanganya kila uchao kuwa mko sawa wakati anahubiri na kufanya ubaguzi si muuza fisi nawe mnunua na mla fisi? Ufisi ni kulana kama wafanyavyo fisi.
Fisi kwa uroho wake aweza kula nyama ya fisi mwenzake. Je, wala rushwa si mafisi wala fisi? ufisadi nao unauweka kapu gani? Nambie na urongo na usanii si ufisi. Je, matapeli wa kidini hata kisiasa na kiuchumi si wauza fisi na mafisi wala fisi? Yeyote aweza kufa fisi isipokuwa mimi muotaji. Tuonane baadaye nikiamka. 
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 11, 2012

No comments: